Sita wakamatwa kupanga kumshambulia Macron

Sita wakamatwa kupanga kumshambulia Macron

Like
451
0
Thursday, 08 November 2018
Global News

Maafisa wa usalama nchini Ufaransa wamesema wamewakamata watu sita wanaoshukiwa kupanga njama za kumshambulia rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron

Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema maafisa wa ujasusi wanawashikilia washukiwa hao sita katika maeneo matatu tofauti, mmoja akiwa maeneo ya milima ya Alps, Mwengine Brittany na washukiwa wengine wanne wakizuiliwa karibu na mpaka wa Ubelgiji na Ufaransa mjini Moselle.

Mpango huo wa kumlenga rais wa Ufaransa ulionekana kutokuwa dhahiri na usiokamilika, lakini ulikuwa ni wa vurugu alisema afisa huyo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Christophe Castaner

Serikali ya Ufaransa imesema washukiwa waliokamatwa ni kati ya miaka 22 na 62 na kumjumuisha mwanamke mmoja.

Akizungumza na waandishi habari Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Christophe Castaner amesema washukiwa hao wanaaminika kuwa wanaharakati wanaoegemea siasa kali za mrengo wa kulia, na kwamba kwa sasa kuna hofu ya kupokea vitisho kutoka kwa kundi hilo.

“Bila shaka nafahamu juu ya tukio hili, siwezi kulipuuza lakini bila shaka linahusiana na mtandao unaofungamanishwa na siasa kali za mrengo wa kulia,  ambao kwa muda sasa umekuwa ukipata nguvu na kuzusha vurugu. Uchunguzi uko wazi na kuanzia sasa utaendeshwa na mahakama,” alisema waziri Castaner.

Mpango wa kushambulia wagundulika wakati mipango ya kuadhimisha kumalizika vita vya kwanza vya dunia ikiendelea.

Marais wa Ufaransa wamekuwa wakilengwa mara  kwa mara katika miongo kadhaa iliyopita. Mwaka 2002 mwanachama wa mrengo huo wa kulia alijaribu kumshambulia rais wa wakati huo Jacques Chirac katika mtaa mashuhuri wa Champs-Elysees mjini Paris wakati wa sherehe za kitaifa za Bastille.

Hayo yalijiri wakati rais Emmanuel Macron akiwa katika mji mmoja Kaskazini Mashariki wa Verdun jana, akihudhuria sherehe za kuadhimisha kumalizika kwa vita vya kwanza vya dunia.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Mpango huo wa kumshambulia rais huyo wa Ufaransa, uligundulika siku kadhaa kabla rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wengine wa dunia kuwasili nchini Ufaransa mwishoni mwa juma hili kuadhimisha miaka 100 ya kumalizika kwa vita hivyo vya kwanza vya dunia hapo Novemba 11.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *