Serikali yatishia kufuta leseni za wafanyabiashara wa korosho

Serikali yatishia kufuta leseni za wafanyabiashara wa korosho

Like
497
0
Friday, 09 November 2018
Local News

Sakata la korosho nchini  lianendelea kufukuta na sasa serikali ya nchi hiyo imewapa wafanyabiashara siku nne za mwisho kununua zao hilo.

Kikao cha Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kati) na Waziri wa Kilimo Charles Tizeba pamoja na wafanyabiashara Septemba 28 kilitazamiwa kumaliza sakata la ununuzi

Siku 11 zilizopita, Rais John Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walikutana na wanunuzi wa zao hilo baada ya kutokea mgomo wa wakulima kuuza korosho zao kwa wanunuzi hao.

Mwaka jana zao hilo liliuzwa kwa wastani wa Shilingi 4,000 kwa kilo lakini mwaka huu bei ikaporomoka mpaka wastani wa Sh1,900 mpaka Sh2,700 kwa kilo.

Mgomo wa wakulima hao uliungwa mkono na Serikali ambapo tarehe 28 Septemba kwenye kikao baina yao na Magufuli na Majaliwa wafanyabiashara hao walikubali kununua zao hilo kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.

Serikali pia ilikubali kwa upande wake kuondosha baadhi ya tozo na vikwazo vilivyopelekea wafanyabiashara kushusha bei.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wanaounda kampuni 35 wanaripotiwa kutonunua korosho hiyo kama ilivyotarajiwa na hali hiyo imechukuliwa na serikali kama mgomo baridi.

Leo hii Waziri Mkuu Majaliwa amekuja na onyo la mwisho; waseme ndani ya siku nne zijazo watanuanua tani ngapi na lini ama wafutiwe leseni zao za biashara.

“Hivyo wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidodo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24,” amesema Majaliwa.

“Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua wakionesha kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.”

Katika kikao cha Septemba 28, Rais Magufuli alinda mbali kwa kuwaambia wafanyabiashara hao kuwa serikali yake ipo radhi kuzinunua korosho zote kwa bei inayowafaa wakulima na kuziuza katika masoko ya kimataifa nchini Marekani na Uchina.

Rais Magufuli amesema yupo tayari kutumia jeshi kununua korosho kwa bei ambayo inakubalika na wakulima.

“…nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri” amesisitiza Rais Magufuli.

Jana Alhamisi Majaliwa alitangaza bungeni kuwa serikali pia inajadiliana na wanunuzi kutoka nje ya nchi ili kuwavutia kununua zo hilo ambalo ndilo mhimili mkuu wa kiuchumi kwa wakaazi wa mikoa ya kusini mwa.

Wafanyabiashara wa korosho wakimsikiliza Rais Magufuli Septemba 28

Mapema mwezi Mwezi Juni mwaka huu kulikuwa na mnyukano bungeni ambapo wabunge bila kujali tofauti zao za kisiasa walikuwa wakiyapinga mapendekezo ya serikali katika Sheria ya Fedha wa mwaka 2018 kwa kuchukua asilimia 100 ya tozo za mauzo ya korosho nje ya nchi (Export levy) kupelekwa mfuko mkuu wa fedha za serikali.

Awali, asilimia 65 ya tozo hiyo ilikuwa ianenda kwenye mfuko wa zao hilo na baadae kurejeshwa kwa wakulima kupitia pembejeo. Hoja ya wabunge wakiongozwa na kamati ya bajeti ilikuwa, hatua ya kuchukua fedha zote ingeleta athari kubwa kwa maendeleo ya zao hilo na wakulima wake.

Mjadala ukawa mkali lakini hoja ya serikali ikapita. Baadae, Rai John Magufuli akasema hakupendezwa na namna ya wabunge wa CCM hususani wa mikoa ya kusini kwa namna walivyolijadili suala hilo, na akatishia kuwa laiti wangeliandamana basi angetuma askari wawaadhibu.

Msimu wa mwaka jana, serikali iliingiza kiasi cha dola 209 milioni za Marekani kutokana na zao la korosho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *