Uchaguzi Zimbabwe: Ghasia zazuka kati ya upinzani na maafisa wa usalama

Uchaguzi Zimbabwe: Ghasia zazuka kati ya upinzani na maafisa wa usalama

Like
330
0
Thursday, 02 August 2018
Global News

Ghasia zimezuka nchini Zimbabwe kati ya wafuasi wa upinzani na vikosi vya
usalama katika mji mkuu wa Zimbabwe huku kukiwa na maandamano dhidi
ya kucheleweshwa kwa matokeo ya uchaguzi
Magari yaliobeba maji ya kuwatawanya waandamanaji na vitoa machozi
yalitumiwa katika barabara muhimu za mji wa Harare baada ya wafuasi wa
chama cha upinzani cha MDC Alliance kuweka vizuizi katikati ya mji huo.
Mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji ameuawa kwa kupigwa
risasi na polisi. Muungano wa Ulaya umeonyesha wasiwasi wake kuhusu
kucheleweshwa kwa matokeo.
Maandamano hayo ya wafuasi wa chama cha upizani cha MDC mjini Harare
yalibadilika na kuwa mabaya nyakati za mchana.
Makundi ya waandamanaji yalikuwa katikati ya mji huo tangu alfajiri lakini
habari zilipozuka kwamba Zanu Pf imeshinda viti vingi katika bunge na
kwamba matokeo ya urais hayakuwa tayari , hali ilibadilika.
Walifanya maandamano katika barabara muhimu mjini Harare na kuelekea
katika ofisi za zamani za chama cha Zanu Pf wakibeba mawe makubwa , fimbo
na chochote kila ambacho wangeweza kubeba.
Kundi hilo lilisema 'tunamtaka Chamisa', wanaamini kwamba uchaguzi huo
umekumbwa na udanganyifu na sasa wanataka mgombea wa MDC
kutangazwa mshindi.
Matokeo yanaonyesha kwamba Zanu-PF inashinda viti vingi vya ubunge
katika uchaguzi huo tangu kung'atuliwa madarakani kwa Robert Mugabe
Matokeo ya kura ya urais yanatarajiwa baadaye siku ya Jumatano.
Mapema , chama cha upinzani cha MDC Alliance kilikuwa kimesema kwamba
kura hiyo ilifanyiwa udanganyifu na kwamba mgombea wake Nelson Chamisa
alikuwa ameibuka mshindi.

Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe Zec imetangaza kwamba Zanu Pf kufikia
sasa imejishindia viti 110 huku MDC ikijipatia viti 41 kulingana na chombo
cha habari cha ZBC.
Kuna viti 210 katika bunge la taifa hilo.
Uchaguzi wa Jumatatu ulivutia asilimia 71 ya wapiga kura. Chombo cha habari
cha ZBC kimesema kuwa Zec itatangaza matokeo ya uchaguzi wa urais
mwendo wa 12.30 za Zimbabwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *