Viongozi watofautiana kuhusu kura ya maoni ya katiba Kenya

Viongozi watofautiana kuhusu kura ya maoni ya katiba Kenya

Like
1429
0
Monday, 08 October 2018
Global News

Wanasiasa kutoka nchini Kenya wameendelea kushinikiza hoja ya mabadiliko ya katiba ila kwa lengo kupunguza gharama ya serikali.

Aliyekuwa waziri mkuu nchini humo Raila Odinga amekuwa akitoa wito wa kura ya maoni kuhusu katika ili kuongeza nafasi za uongozi na kuwa na serikali yeney uwakilishi zaidi.

Ni mjadala wa kitaifa ambao umeibua maoni mseto miongoni mwa viongozi na wanasiasa.

Wanaounga mkono kura ya maoni ya kubadilisha katiba ya mwaka 2010, wanasema watafanya hivyo kwa masharti kwamba itapunguza gharama ya oparesheni za serikali na kuletea wananchi manufaa ya moja kwa moja.

Seneta wa zamani Boni Khalwale, anaona kuwa kubadilisha katiba ili kuwa na nafasi zaidi za viongoni serikalini ni kuongeza mzigo wa ushuru kwa wananchi.

“Ukiunda ofisi ya waziri mkuu, naibu wa waziri mkuu, Rais na manaibu wa rais wawili, itamaanisha utakuwa umeongeza gharama ya kuongoza nchi mara nyingi ”

Lakini pia baadhi ya viongozi wanaona kuwa kupunguza nafasi za uwakilishi kwenye bunge au kaunti kutawanyima fursa na huduma za serikali baaadhi ya wananchi.

Aden Duale ni kiongozi wa wengi bungeni.

Ni mbunge anayewakilisha eneo kame la wafugaji kaskazini mwa Kenya ni kiongozi wa kundi la wabunge kutoka kanda ya wafugaji.

Anaunga mkono kuwepo na kura ya maoni lakini anapinga mabadiliko yanayoweza kuathiri jamii yake.

“sisi kama wafugaji tunataka mabadiliko ya katiba na tunaomba rais aite mkutano wa wabunge ili tukubaliane kila kitu. Tukubaliene maswala ya wafugaji wa kaskazini Mashariki kwa sababu hatuwezi kukubali eneo hata moja la uwakilishi bungeni katika kanda ya wafugaji liondolewe”

Mjadala wa kutaka kuwepo na kura ya maoni unaongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Anaona kwamba kwa kubadilisha katiba na kuwa na nafasi nyingi za uongozi kutasaidia kuleta usawa kwa jamii zote na kuhakikisha kila mkenya amewakilishwa.

Odinga amependekeza katiba ifanyiwe mabadiliko ili kubuniwa ngazi tatu za utawala, akisema hatua hiyo itafanikisha ugavi wa sasa wa rasilimali na kufanikisha malengo ya ugatuzi.

Anapendekeza pia kubuniwa kwa maeneo 14 zaidi ya utawala huku serikali 47 za kaunti zikiendelea kudumishwa kama ilivyo sasa.

Pia anasema mabadiliko ya katiba ni sehemu ya makubaliano yake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Mimi nataka kuona mema kwa wakenya wote na ile tume tumeunda itazunguka Kenya yote kutafuta maoni ya wakenya vile wanataka kuboresha utawala katika nchi yetu na wakenya wakipendekeza tupige msasa katiba yetu basi hakuna ubaya”

Na haya ni maoni ya wakenya kuhusu kura hiyo ya maoni

Iwapo hatimaye kenyaitapiga kura ya maoni kuhusu katiba basi itakuwa ni mara ya tatu kufanya hivyo, baada ya ile ya mwaka 2005 na 2010.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *