Category: Local News

  • Lukuvi aanza na bibi aliyemlilia Maguful

    Lukuvi aanza na bibi aliyemlilia Maguful

    Kilio cha Nyasasi Masige, mkazi wa Bunda mkoani Mara mbele ya Rais John Mgufuli kuhusu kuwapo kwa njama za kudhulumiwa ardhi yake, kimezaa matunda baada ya waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutua wilayani humo na kumaliza mgogoro huo.

    Waziri Lukuvi anayetembelea Mkoa wa Mara kutatua migogoro ya ardhi na kutekeleza agizo la Rais Magufuli, jana aliwaagiza watendaji wa idara ya ardhi mkoani humo kushirikiana na wenzao wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kupima upya eneo la Nyasura ‘C’ ilipo ardhi ya bibi huyo na wamgawie viwanja viwili kama njia ya kumaliza mgogoro huo.

    Septemba 5, 2018, kikongwe huyo alilalamika mbele ya Rais Magufuli kuwa baadhi ya watu akiwamo tajiri mmoja wilayani Bunda kwa kushirikiana na wataalamu wa idara ya ardhi walikuwa na njama za kumdhulumu ardhi yake, hali iliyofanya kiongozi huyo mkuu wa nchi kumwagiza Waziri Lukuvi kufika Mara kushughulikia migogoro ya ardhi.

    Akizungumza muda mfupi baada ya kumsikiliza bibi huyo, Lukuvi alisema amegundua kuwapo nia ovu wakati wa upimaji na uandaaji wa michoro ya eneo la Nyasura ‘C’.

    “Haiwezekani eneo moja kukawepo na viwanja vyenye ukubwa tofauti kama ilivyokuwa katika eneo hili. Inaonyesha haya (makosa) yalifanyika makusudi kwa manufaa ya baadhi ya watu,” alisema Lukuvi.

    Akionyesha kukerwa na makosa aliyoyagundua, waziri huyo aliagiza kazi ya kupima na kuweka michoro upya ya eneo hilo ifanyike na kukamilika ifikapo kesho.

    “Mtengeneze mchoro mpya na mpime upya eneo hili na bibi kizee huyu apewe viwanja viwili bila kutozwa tozo ya premium ya asilimia 2.5 ya thamani ya ardhi kwa sababu hana uwezo. Zingatieni sheria kutekeleza hilo kwa kuhakikisha viwanja vyote vinalingana na nyumba yoyote isibomolewe,” aliagiza.

    Mmoja wa wakazi wa eneo la Nyasura ‘C’, Laban Ndege aliyelalamikiwa na bibi huyo kutaka kumpora ardhi yake, alikubaliana na uamuzi wa waziri na kutumia fursa hiyo kuwasilisha malalamiko yake ya kutopewa hati ya kiwanja licha ya kukamilisha taratibu zote pamoja na malipo.

    Taarifa hiyo ilimfanya Lukuvi kuwahoji watendaji wa idara ya ardhi na kugundua kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawajapewa hatimiliki za ardhi licha ya upimaji kufanyika zaidi ya miaka 10 iliyopita.

    Akizungumzia migogoro ya ardhi mbele ya waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alisema migogoro na kero nyingi za ardhi wilayani humo zinachangiwa na utendaji usioridhisha wa mabaraza ya ardhi ya kata.

    Pamoja na kufanya kazi kinyume cha sheria na utaratibu, mkuu huyo wa wilaya pia aliyatuhumu mabaraza hayo kufuata mila na desturi za wenyeji ambazo nyingi ni kandamizi dhidi ya haki za wanawake.

  • Tanzia: CCM Yapata Pigo, Guninita Afariki Dunia

    Tanzia: CCM Yapata Pigo, Guninita Afariki Dunia

    ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Taifa na baadaye akawa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita amefariki dunia leo Alhamisi, Septemba 13, 2018 alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

    Taarifa za msiba huo zimethibitishwa na mdogo wake na marehemu, Gerald Guninita ambaye naye aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo wakati wa Uongozi wa Awamu ya Nne.

    Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja Muhimbili, Aminiel Aligaesha amesema kwamba, Guninita amefariki dunia leo saa 12 asubuhi na alilazwa Muhimbili tangu Septemba 6, mwaka huu.

    Mnamo Agosti 14, 2015, John Guninita na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja walihamia Chadema wakati wa vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka huo lakini baadaye Guninita alirejea tena CCM.

  • MENEJA SIMBA AFUNGIWA  MWAKA MMOJA NA TFF KUJIHUSISHA NA SOKA, FAINI

    MENEJA SIMBA AFUNGIWA MWAKA MMOJA NA TFF KUJIHUSISHA NA SOKA, FAINI

    Meneja wa Simba SC, Robert Richard amefungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa muda wa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka huku adhabu hiyo ikiambatana na faini ya shilingi za Kitanzania, milioni 4.

    Adhabu hiyo imetolewa kutokana na kosa la kuihujumu timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

  • TUMENUFAIKA NA MKUTANO WA  FOCAC-MAJALIWA

    TUMENUFAIKA NA MKUTANO WA FOCAC-MAJALIWA

    WAZIRI MKUUKassim Majaliwa amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa kutokana na kushiriki kwake katika Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

     

    Amesema kikao hicho kimekuwa na tija kwa Tanzania kutokana na maeneo ya vipaumbele yaliyojadiliwa katika mkutano huo hususani masuala ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

     

    Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumatano, Septemba 05, 2018) alipokutana na waandishi wa habari katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi China ambako alikwenda kumuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye mkutano wa FOCAC.

     

    Alisema maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mkutano huo ni masuala ya usalama wa nchi, maendeleo ya kiuchumi hususani uboreshaji wa sekta ya viwanda, elimu, kilimo, afya, elimu na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

     

    “Kikao hiki kimekuwa na tija kwa Tanzania kwa sababu maeneo yote yaliyojadiliwa ni muhimu kwetu. Tumeanza kuona idadi nzuri ya wawekezaji kutoka China na ni matokeo ya mpango uliowekwa katika kikao cha kwanza cha FOCAC kilichofanyika Afrika Kusini.”

     

    Waziri Mkuu alisema maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na sekta ya madini, mifugo na uvuvi, ambazo nazo zimewekewa mikakati ya namna ya kuziboresha ili ili ziweze kuchangia ukuzaji wa uchumi katika mataifa hayo.

     

    Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kikao hiko pia kilijadili namna ya kuboresha sekta ya utalii kwa kuvutia watalii kutoka za Afrika na nje ya bara hilo ikiwemo na China, hivyo Tanzania inatakiwa kutumia fursa fursa zilizopo kuvutia watalii kutoka nchi mbalimbali.

     

    Alisema ushirikiano huo unaanza mara moja na China imetenga dola bilini 60 za Marekani kwa ajili ya kusaidia Afrika ili ziweze kuboresha maeneo hayo yaliyoainishwa. Tanzania inatakiwa kutumia vizuri fursa hiyo.

     

    Pia Waziri Mkuualisema atakaporejea nchini ataitisha kikao cha kazi cha Mawaziri na kutoa maelekezo kwa mawaziri wote ambao sekta zao zimeguswa  kwenye mpango wa FOCAC ili waweze kuandaa utaratibu mzuri wa namna tukavyonufaika na fedha hizo.

    “Watanzania tushirikiane kwa pamoja na watendaji katika wizara zote ili tuweze kujipanga vizuri. Wataalamu katika kila sekta waweke mpango kazi utakaokwenda kuhitaji fedha hizo kwa ajili ya kuimarisha sekta husika ili maeneo yote yapate tija.”

     

    Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Rais wa China, Xi Jinpingkwa kuitambua Tanzania kama moja kati ya nchi rafiki wa muda mrefu wa China na kuipa kipaumbele kwenye mkakati wa kuwekeza kwenye viwanda.

     

    Alisema wawekezaji wengi kutoka China wamedhamiria kuja Tanzania kujenga viwanda na kuviendesha kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ili viweze kuzalisha kwa uhakika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

     

    Waziri Mkuu alisema tayari Tanzania ilishafanikiwa katika mkakati wa kuboresha mazao makuu matano ya biashara ambayo ni korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku na sasa imejipanga kuboresha mazao ya mbegu za kuzalisha mafuta na ameitaka mikoa husika ifuatilie mazao hao ambayo ni michikichi, alizeti na ufuta.

     

    Mkutano huo wa FOCAC wa siku mbili ulifunguliwa Jumatatu, Septemba 03, 2018 jijini Beijing China na Rais wa China, Xi Jinping. Ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi 53 kutoka Afrika.

     

     

    (mwisho)

     

    IMETOLEWA NA:

    OFISI YA WAZIRI MKUU,

    ALHAMISI, SEPTEMBA 06, 2018.

  • Msafara wa Rais Magufuli wapata ajali Mara

    Msafara wa Rais Magufuli wapata ajali Mara

    MSAFARA wa Rais John Magufuli uliokuwa ukielekea wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, umepata ajali katika kijiji cha Kasuguti, kata ya Kisorya, wilayani Bunda mkoani Mara, leo Septemba 4, 2018 baada ya magari manne kugongana katika eneo ambalo barabara ilikuwa ikijengwa.
    Taarifa za awali zinadai kuwa waandishi wawili wa habari wamejeruhiwa baada ya gari walimokuwa kupinduka.
    Amesema chanzo cha ajali hiyo ni vumbi lilikuwa limetapakaa barabarani kutokana na msafara huo hivyo madereva kushindwa kuona vizuri njia lakini hakuna madhara makubwa licha ya gari moja kubondeka ubavuni baada ya kupinduka.
    Majeruhi wa ajli hiyo ni watu wawili ambao ni Neema Emmanuel, waandishi wa Gazeti la Nipashe ambaye ameumia kichwani na Tunu Heriman ambaye alipata mshituko tu lakini kwa sasa wote wanaendelea vizuri

  • Tunatoa Pole kwa Mama Mzazi wa Mbunge ‘Sugu’ Ambaye Amefarik Dunia Jana

    Tunatoa Pole kwa Mama Mzazi wa Mbunge ‘Sugu’ Ambaye Amefarik Dunia Jana

    Mama mzazi wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (CHADEMA), amefariki dunia jana Jumapili Agosti 26, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu.

    Uongozi wa TV E na EFM Redio unatoa pole kwa Mbunge Sugu pamoja na Familia yake, Mungu hawaongoze kwenye kipindi hiki Kigumu.

     

  • Lugola amuagiza DCI amkamate aliyekuwa mkurugenzi Nida

    Lugola amuagiza DCI amkamate aliyekuwa mkurugenzi Nida

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemuagiza Mkurugenzi wa Makosa Jinai nchini (DCI) kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu kabla ya saa 12 jioni leo na tayari ameshakamata na kupelekwa Dar es Salaam.

    Lugola pia ameagiza kukamatwa kwa wamiliki wa kampuni tatu zinazodaiwa kuhusika katika mradi wa vitambulisho vya taifa, Gotham’s International Limited, Gwiholoto Impex Ltd na Aste Insurance wanaodaiwa kufanya udanganyifu na kushindwa kurejesha fedha walizotumia kinyume na utaratibu.

    Akizungumza na wanahabari leo Agosti 21, Lugola ameagiza kukamatwa watumishi wote wa Nida ambao wanatuhumiwa katika ubadhirifu wa fedha za umma wakishirikina na kampuni hizo. “Hizi kampuni zimefanya udanganyifu zikishirikiana na baadhi ya wafanyakazi,”amesema.

    Hata hivyo amesema baadhi ya kampuni zilizohusika na ubadhirifu huo zimeanza kurejesha fedha za umma kwa asilimia 84.

  • Rais wa Uganda Museveni anakanusha kwamba Bobi Wine amejeruhiwa

    Rais wa Uganda Museveni anakanusha kwamba Bobi Wine amejeruhiwa

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekanusha kwamba mbunge wa upinzani Bobi Wine amejeruhiwa.

    Katika taarifa yake ya kwanza kuhusu afya ya mbunge huyo aliyekamatwa na vikosi vya usalama nchini, Museveni amevishutumu vyombo vya habari kwa kile alichokitaja ni kueneza habari zisizo za kweli kuhusu suala hilo.

    Kulingana na ripoti mbalimbali za vyombo vya habari mbunge huyo ambaye pia ni msanii, Robert Kyagulanyi ana matatizo ya figo ambayo yanahitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea katika kutiba sehemu nyeti kama hizo za ndani ya mwili.

    “Vyombo vya kueneza habari zisizo za kweli vimekuwa vikitangaza kwamba mjukuu wetu, asiye na nidhamu Bobi Wine, ni mgonjwa mahututi, hawezi kuzungumza na mengineyo.

    “Wamekuwa wakisema kuwa huenda maafisa wa usalama wamemjeruhi vibaya Bobi Wine kwasababu ya namna walivyokabiliana na wabunge wakati wakiwakamata.

    “Nimeamua kuwasiliana na madaktari wa jeshi, kwasababu ya nidhamu ya jeshi, madaktari wa UPDF daima wanachukua tahadhari katika hali kama hizi. Tayari Bobi Wine alionekana na madaktari Arua, Gulu na Kampala. Hakuwa na majeraha ya kichwa, kifua au mifupa kuvunjika, wameniarifu,” ilisema taarifa ya rais.

    Kadhalika Museveni alilaumu watu maalum ambao alieleza kuwa ni wa nje wanaotafuta kuingilia siasa za nchi hiyo.

    Chama cha wafanyakazi wa afya nchini Uganda kinasema mahali wanapohifadhiwa wabunge wa upinzani na vyombo vya usalama akiwemo Bobi Wine ni ya hatari na inaweza kuwasababishia vifo.

    Viongozi wa chama hicho wamesema madaktari wa Jeshi la UPDF hawana ujuzi wa kutosha kuwafanyia matibabu wabunge hao wanaodaiwa kujeruhiwa vibaya na maafisa wa usalama.

    Wameelezea kuwa wako tayari kushirikiana na UPDf kuwashughulikia wabunge hao na washukiwa wengine kufuatia ghasia hizo.

    Daktari Edward Ekwaro Ebuku, rais wa chama cha wafanyakazi wa afya Uganda ameeleza, ‘Ugonjwa wa figo unatakiwa uangalizi wa dharura, jeshi la Uganda limemficha huyu Bobi Wine, isitoshe walimkataza Daktari wa familia kumtibu’.

    ‘Sasa hivi hatujui hali yake ikoje. Lakini tunafikiria wamemficha kwasababu hali yake ni mbaya zaidi’.

    Wataalamu wa afya wanafafanua kuwa mtu akiwa na matatizo kwenye figo ni rahisi sana sehemu zingine kama maini na ubongo wake kuathirika iwapo hatua za dharura hazichukuliwi kumtibu.

    Wameongezea kuwa mbunge Francis Zake ambaye ni miongoni mwa waliokamatwa yuko katika hali mahututi na anahitaji kuhamishwa kutoka hospitali moja hadi nyingine kupata matibabu ya hali ya juu.

    Wamejitolea kushirikiana na UPDF kutoa matibabu ili kuyanusuru maisha ya wahanga wote wa ghasia waliojeruhiwa na waliomo katika hali mbaya.

    ‘Hatujapata ruhusa kuingia kambi za jeshi pahali hawa wabunge wa Uganda, tutamuandikia mkuu wa jeshi rais Yoweri Kaguta Museveni ili atupe ruhusa twende tumsaidie huyu mheshimiwa Robert Kyagulanyi’ amesema Ebuku.

    Hapo jana mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na wengine watano kupata majeraha wakati polisi ilipokuwa ikizima maandamano ya wakaazi wa Manispaa ya Mityana magharibi mwa Kampala.

    Vurugu hizo ziliibuka baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa mbunge wa upinzani Francis Zaake amekufa baada ya kupigwa na maafisa wa usalama anakoshikiliwa yeye na wenzake.

    Waganda walioko nje wameendelea kutuma ujumbe wa kuishtumu serikali kwa vitendo vyake vya kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani na raia kwenye mitandao ya kijamii.

    Katika mji wa Toronto nchini Canada maandamano makubwa yalifanyika kwenye barabara za mji huo siku ya Jumamosi huku raia wengine nao walituma kanda binafsi za video kutoka Afrika Kusini na Marekani.

  • Hali ya Kingwalla Yazidi Kuimarika

    Hali ya Kingwalla Yazidi Kuimarika

    HALI ya Waziri wa Maliasili na Utali, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla imeendelea kuimarika vizuri kutokana na matibabu anayopatiwa katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili alikolazwa baada ya kupata ajali ya gari akiwa mkoani Arusha kuelekea Dodoma kikazi.
    Picha zinaonesha Kigwangalla akiwa amepata nafuu na kutoka nje ya Jengo la Hospitali hiyo jambo linaloonyesha faraja huenda akapona hivi karibuni.
    Mbunge huyo wa Nzega (CCM) alipata ajali wiki chache zilizopita baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Afisa habari wake, Hamza Temba aliyezikwa mkoani Tanga.
  • Biteko atoa wiki moja kwa muwekezaji kulipa kodi ya madini serikalini

    Biteko atoa wiki moja kwa muwekezaji kulipa kodi ya madini serikalini

    Naibu waziri wa madini, Dotto Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo wa eneo la Kilalani, baada ya kutembelea eneo hilo.
     
     
    Serikali imempa muda wa wiki moja nwekezaji mmiliki wa kampuni ya Amazon Trading (T)Company Limited Abdi Hozza kuhakikisha anailipa serikali kodi ya pango ya uwekezaji kiasi cha dola za Marekani 70,020 sawa na zaidi ya shilingi milioni 140 za kitanzania anazodaiwa tangu mwaka 2011 katika machimbo ya Kalalani eneo la Umba wilayani Korogwe kutokana na leseni nane za uchimbaji wa madini kuanzialeseni namba (102-109/2001) anazomiliki .
    Sambamba na hilo imeiagiza serikali ya wilaya ya Korogwe kuhakikisha inatenga maeneo ya wachimbaji wadogowadogo wa madini ili kuepusha migogoro iliyodumu kwa muda mrefu hali ambayo imeleta hali ya chuki baina ya mwekezaji na wananchi.
    Waziri Biteko alitoa agizo hilo alipotembelea katika machimbo hayo juzi Jumamosi katika vijiji vya Kigwasi na Kalalani kata ya Kalalani wilayani humo. Biteko alimtaka ndani ya wiki moja mwekezaji huyo kulipa kodi hiyo ya pango anayodaiwa na serikali na amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuwabaini wageni na watu wanaonunua madini kwa njia za panya.
    Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, akikagua Mabaki ya mgodi wa Amazon,ambao umesitisha uchimbaji kwa miaka mingi kutokana na Matatizo mbalimbali.
     
    “Haiwezekani tangu madini yaanze kuchimbwa katika machimbo haya serikali haijapata kodi kutokana na mgodi huu tunakuta sifuri nimewaambia wailipe haraka nataka nikifika Dodoma kuna commitment statement mnalipa lini” alisema.
    Aliongeza “Na yule anayedhani atakuja Kalalani kununua madini kwa njia ya panya muda huo umekwisha,na tumekwenda kwenye mto tumekuta mnachimba madini,sheria inakataza kuchimba madini kwenye vyanzo vya maji naomba kuanzia sasa mkaondoe vifaa vyenu kule mtoni”.
    Aidha Waziri Biteko, aliongeza kuwa eneo hilo la Kalalani lina leseni za wachimbaji wadogo wa madini ya vito zipatazo 400 lakini leseni zilizohai na zinaendelea kufanya kazi ya uchimbaji ni 70 tu kati ya hizo. Awali diwani wa kata hiyo Amati Ngerera alimueleza naibu waziri kuwa mwekezaji huyo(Amazon)hana mahusiano mazuri na wa wanakijiji pamoja na wachimbaji wadogowadogo wa hapo kutokana baada ya
    kupewa leseni na serikali kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo alilitelekeza kwa muda mrefu bila ya kuendeleza shughuli zozote na wananchi wengi ambao shughuli zao kubwa ni uchimbaji waliokuwa wakiingia eneo hilo walifanyiwa vitendo vya visivyokuwa vya kibinadamu ikiwemo kupigwa risasi,kubakwa na askari aliowaweka kulinda eneo hilo.
    Diwani huyo alikwenda mbali zaidi kuwa mwekezaji huyo huwa anatumia eneo hilo kama dhamana ya kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha na alimpa mwenzake anaitwa Najim kuendesha mgodi huo kinyemela bila ya serikali kuwa na taarifa.
    “Huyu mwekezaji leseni yake ilikwisha tangu mwaka 2001,wananchi wakaomba leseni ya uchimbaji na yeye akaomba ,lakini baadae akaingia mkataba na mfanyabiashara anayeitwa Najim halafu yeye akajitoa kabisa na huyo Najim hachimbi bali anafanya shughuli zake za biashara ya utalii na huyu Amazon anatumia eneo hili kukopea fedha kwenye taasisi za fedha ”alisema.
    Aliongeza “Serikali ya kijiji ilifanya mapendekezo matatu na kuyapeleka katika baraza la madiwani na baadae tukayandika kuyaleta katika ofisi yako,mapendekezo haoy ni eneo hilo litafutwe mwekezaji mwenye sifa ya uwekezaji,nyumba zilizopo eneo la mgodi zirudishwe serikalini ambazo waasisi wake ni STAMICO na wananchi wakatiwe eneo ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi za uchimbaji”.
    Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwasi, Loronyotu Lakaney alimueleza Naibu Waziri kuwa mbali na mgodi huo kutelekezwa na mwekezaji huyo pia madini yanatorosha kwa njia za panya na kuuzwa Voi nchini Kenya.
    “Mheshimiwa Naibu waziri mbali na mgogoro huo pia wachimbaji wengi wadogowadogo wakishapata madini wanakwenda kuyauza Voi mpakani mwa Kenya na Tanzania upande wa hapa Tanga kutokana hakuna udhibiti na hakuna minada ya madini inayoendeshwa kama serikali ilivyoagiza”alisema.
    Naye mwekezaji huyo alimueleza Naibu waziri kuwa alichelewa kulipa hiyo kodi kutokana Kutokupewa taarifa yoyote ya kuendeleza mgodi wala kudaiwa kodi.
    “Mheshimiwa Naibu waziri mimi ni kweli kwa muda mrefu sijapaendeleza hapa baada ya leseni yangu kwisha mwaka 2011 sijapewa leseni nyingine wala sijapata hiyo barua ya kulipa hiyo kodi ya pango”alisema.
    Taarifa ya ofisi ya Afisa Madini Mkazi mkoa wa Tanga amabayo gazeti hili inayo nakala yake ilishapendekeza kwa kamishna wa madini leseni hizo nane za mwekezaji ziandikiwe hati ya makosa(default notice) na hatimaye zifutwe kwa mujibu wa sheria ya madini mwaka 2010,lakini kwenye mfumo wa flexicadastre leseni hizo zinaonesha zipo hai(active in default) ingawa zilishaisha muda wake tangu Septemba 30,2011.
  • RC MAKONDA AVIWEZESHA KIUCHUMI VIKUNDI VYA JOGGING KWA KUVIPATIA MITAJI

    RC MAKONDA AVIWEZESHA KIUCHUMI VIKUNDI VYA JOGGING KWA KUVIPATIA MITAJI

    Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ameanza rasmi mpango wa kuviwezesha kiuchumi vilabu vya Jogging kwa kuvipatia mitaji ya kuwezesha kuanzisha miradi ya kujikwamua kiuchumi.

    Akizungumza wakati wa Bonanza la Vilabu vya Jogging Dar es salaam RC Makonda ameanza kwa kukabidhi kitita cha zawadi ya shilingi milioni 10 kwa washindi wa makundi mbalimbali pamoja na kuahidi kukabidhi shilingi Million Saba kwa chama cha Jogging Temeke ili waweze kuwa na SACOS yao endapo atajiridhisha kuwa wamekidhi vigezo.

    Aidha RC Makonda amesema anachokitaka kwa sasa ni kuona vilabu vya Jogging vinashiriki shughuli za uzalishaji Mali ili wajikwamue kiuchumi na wasipate muda wa kushiriki matukio ya uhalifu kama uporaji, ubakaji na matumizi ya dawa za kulevya.

    RC Makonda amesema kila baada ya miezi miwili yatakuwa yakifanyika mabonanza makubwa ya Jogging hivyo amezitaka kila wilaya kujiandaa.

    Pamoja na hayo RC Makonda amewataka vijana mkoani kwake kuchangamkia fursa zote halali zinazopatikana Dar es salaam kwakuwa mkoa huo Ndio chimbuko la mafanikio kwa wengi huku akiwahimiza kumtanguliza Mungu kwa kila jambo.

    Hata RC Makonda hivyo amewaomba Vijana wa Jogging kuwa mstari wa mbele kuwafichua wahalifu ili Dar es salaam iendelee kubaki kuwa jiji lenye amani na usalama wakati wote.

    MICHEZO, AFYA NA UCHUMI.